Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


BARAKAH THE PRINCE, MAPENZI HAYAJAWAHI KUMUACHA MTU SALAMA
Barakah The Prince

Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kunipa pumzi ya kuweza kuzungumza nawe msomaji wangu. Asante kila msomaji ambaye umenitumia maoni na ushauri wake kuhusu Barua Nzito. Barua yangu wiki hii imuendee mdogo wangu na rafiki yangu, Baraka The Prince mzee wa moyo wake. Mdogo wangu uko vizuri, unafanya kazi nzuri sana.

Hivi karibuni Baraka The Prince ulitangaza kujiondoa kwenye Lebo ya Rock Star 4000 na kuamua ‘kujimeneji’ mwenyewe kupitia Lebo ya Bana Music ambayo mmeanzisha wewe na mpenzi wako, Najma ambaye naye ni msanii. Ni jambo jema na zuri, lakini barua yangu inakuhusu wewe Baraka ingawa na Najma itamgusa kwa mbali kidogo.

Kwanza Baraka, tabia yako ya kuhamahama sidhani kama ni sawa, inaonesha wewe ni miongoni mwa wasanii wanaoondoka kwenye lebo bila makubaliano mazuri. Baraka mdogo wangu, hata kabla ya kuondoka kwenye Lebo ya Tetemesha ambayo iko chini ya Kid Bway, tuliwahi kuzungumza na kukushauri kitu kuhusu kutunza heshima ya wale ambao wamekufikisha hapo ulipo, bila kujali kama unahisi unanyonywa au laa. Ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kuzungumza na wewe kuhusu mambo ya muziki na lebo, nikasikia kuwa umeondoka Tetemesha. Nilihuzunika moyoni mwangu kwa sababu Kid alijitoa kukupigania na nakumbuka ndiye alinikutanisha na wewe. Sitaki kuzungumzia mambo yenu na menejimenti yako kwa sababu niliamini nawe ni mtafutaji pengine umeona sehemu nyingine ni bora zaidi.

Lakini kilichonishangaza, ni kusikia tena umeondoka kwenye lebo ambayo uliipata, tena ukaondoka kwa figisufigisu. Nikajifunza kitu hapo, kama haitoshi haikuchukua muda ukahamia tena Rock Star ambayo ni kubwa na inaongoza wasanii wakubwa. Lakini kwa kuwa maji hayajawahi kusahau baridi hata uyachemsheje, hivi karibuni tena umeondoka Rock Star na kuhamia Lebo ya Bana Music ambayo ni muunganiko wa Baraka na Najma ambaye ni mpenzi wako. Kuanzishwa kwa lebo hiyo, ni sahihi na ni hatua lakini najaribu kuiangalia na kuona kama muunganiko wa mapenzi hivi.

Na kwa kawaida mapenzi huwa hayawaachi watu salama. Ninaamini kabisa katika lebo yenu itakuwa mmechangia gharama lakini uwezekanao wa mmoja wenu kutoa gharama kubwa kuliko mwenzake upo pia. Hivi Baraka kama ikitokea, ingawa sikuombei mdogo wangu, viongozi wa Bana mkatofautiana na mmoja wapo akawa anatakiwa kuhamia au kuacha kufanya kazi kwenye lebo, utahamia wapi tena? Kwa sababu kila mtu atakuwa anakuona kama kimeo, anajua utaenda kwake atakufikisha sehemu f’lani hivi, halafu utamuacha solemba.

Bana Music ni lebo ambayo inaongozwa kwa nguvu za mapenzi, vipi kama mkihitilafiana halafu mwenye nguvu kwenye kampuni akasema hakuna upande mwingine kufanya kazi, itakuaje kwa sanaa yako. Bila kujali kama wewe ndiyo mwenye hisa nyingi au mwenza wako.

Jaribu kutafakari na kujiridhisha zaidi kwa kile unachokifanya hasa chini ya mwamvuli wa mapenzi. Mapenzi bwana huwa matamu na mazuri kama mko sawa, lakini mkikoseana na mkashindwa kutumia busara, basi itakuwa kama ya watu wengine ambao wamekuwa wakichambana kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuachana. Najaribu tu kuwafikirisha wadogo zangu Najma na Baraka, ili kuwa makini na kujua nini cha kufanya ingawa hadi hapo mlipofikia ni sehemu nzuri.

Kikubwa kuendelea na nia ya dhati ambayo mmeamua kuwadhihirishia walimwengu kuwa mnaweza kuwa wapenzi na mkafanya kolabo ya jambo fulani na likasimama bila kujali changamoto na magumu ambayo mnayapitia.                    


Facebook Blogger Plugin by

Post a Comment

 
Top