Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


Johari, mume huwezi kumpata kwa matangazo, utachina!
Muigizaji Johari.
BLANDINA Chagula au kama tunavyomfahamu wengi kwa jina la Johari, ni mmoja kati ya waigizaji wa filamu wa kitambo ndani ya Bongo Muvi. Hawa ndiyo wale waburudishaji walioanza sanaa hii wakiwa katika makundi, yeye akiwakilisha kutoka Kundi la Kaole.

Alianza kucheza katika makundi ya maigizo wakati huo ushabiki ukiwa runingani, hadi pale mapinduzi mapya yalipokuja kupitia Filamu ya Girlfriend. Enzi hizo za makundi, wasanii hawa walikuwa ni vipusa walipofanya ziara za kikazi mikoani, kwani walipokelewa kwa nderemo na vifijo kutokana na umahiri wao katika maigizo. Nakumbuka, ilikuwa ni kazi ngumu na kubwa kumfikia msanii kama Johari pale alipo.

Aliendeleza ukali wake hata filamu zilipoanza na haikuwa ajabu yeye kuwa miongoni mwa wasanii wa mwanzomwanzo kabisa kuanzisha kampuni zao za kazi, pale alipoungana na aliyekuwa mpenzi wake wa zamani, Vincent Kigosi ‘Ray’ kuanzisha kampuni yao iliyoitwa RJ. Ni wakati huo ndipo Johari alipokuwa kipusa, akiwasumbua wanaume wakware kwani licha ya ustaa wake, lakini pia alijaaliwa uzuri wa asili, hivyo kumfanya kuwa mmoja kati ya mastaa waliokuwa wakitafutwa zaidi kimapenzi nchini.

Ni wakati huo alipokuwa akiishi kimapenzi na muigizaji mwenzake Ray, lakini pia akihusishwa kutoka na wanaume wengine kadhaa. Ni maisha ya kawaida kwa mastaa wetu, hasa wa kike kuutumia vizuri ujana wao katika kula maisha. Lakini nimejikuta nikipigwa na butwaa siku chache zilizopita, baada ya kumsikia Johari akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini, akisema kwa sasa anatafuta mwanaume wa kumuoa na kama yupo ajitokeze, maana yeye hana neno na wala hana masharti!

Johari akipozi.

Kwanza lazima nimpongeze kwa kufikia hatua ya kuamua kujitoa namna hiyo kuelezea ukweli wake kuhusu kuishi na mume, maana kwa mwanamke kutoa kauli ya kuhitaji mwanaume wa kumuoa, kidogo inaonekana kuwa jambo gumu, hasa kwa mastaa wa hapa nyumbani. Lakini nje ya hapo, naliona tatizo ambalo siyo tu lipo kwa Johari, bali linawakumba mastaa wengi wa kike ambao huwa wapo juu kisanii enzi zao.

Ingawa sina umri kamili wa msanii huyu, lakini nina uhakika ameshavuka miaka 30, umri ambao kwa wanawake kidogo huwa ni kama wamechelewa hivi kuolewa. Na kwa hulka ya wanaume, hasa wa Kibongo, mwanamke anayetangaza kutafuta mume huonekana kama ana matatizo.

Kwa Johari, yeye kama msanii, inaonekana kama baada ya kuzunguka huku na huko akila ujana, baada ya kujihisi sasa muda umekwenda na hakuna mtu mwenye dalili za kuhitaji kumuoa, ameona bora ajitangaze! Huenda alisema vile kama utani au alidhamiria, lakini kitendo cha kukosa mume hadi muda huu, siyo kitu cha kujivunia, hasa kwa msichana mrembo kama yeye.

Heshima ya mwanamke ni kuwa na mume, hayo mengine huwa ni mbwembwe tu. Johari anasimama kwa niaba ya mastaa wengi wa filamu, maana katika eneo hili kidogo afadhali akina dada wa Bongo Fleva, wengi wanaishia katika ndoa wakiwa bado wanavuma.

Hawa wanadanganywa na ustaa, wanaamini huu siyo wakati muafaka wa kuolewa, wakidhani watakosa uhuru ule wanaoutaka. Orodha yao ni ndefu ingawa umri wao nao unakimbia. Pengine ni kutokujua, lakini hakuna kitu kigumu kama ndoa kwa mastaa, kwani wanaume wengi wanawachukulia kama watu ambao hawawezi kuwa waaminifu, hasa kutokana na wingi wa shughuli na mahusiano ya kijamii kati yao na watu wanaowazunguka.

Wakati ule wa kuvuma, ndiyo wakati wa kutengeneza ‘CV’ yako kwa ajili ya maisha ya kinyumba, kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuwa tayari kuoa mwanamke ambaye anafahamika kwa kuwa na utitiri wa wanaume aliotoka nao kabla. Na mwanamke wa kuolewa, kamwe hapigi kelele kwa sababu siku zote mwanaume wa kumuoa huwa yupo tayari!


Facebook Blogger Plugin by

Post a Comment

 
Top