Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


Rais Mstaafu Kikwete na Mkewe mama Salma Kikwete

VIONGOZI wastaafu nchini Tanzania, wakiwemo marais na baadhi ya mawaziri wakuu, sasa wanakomaa na kilimo au ufugaji na mambo mengine ya huduma za kijamii kutekeleza kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, Uwazi limegundua.
Katika uchunguzi uliofanywa na waandishi wetu, imebainika kwamba, mtindo huo wa maisha wameuiga kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alipostaafu mwaka 1985 alirudi kijijini kwake, Butiama mkoani Mara na kujikita kwenye kilimo ambapo alikuwa na ratiba ya kupalilia mahindi yake.
Hata hivyo, uchunguzi huo unaonesha kuwa marais wastaafu, imekuwa si rahisi kwao kwenda kushika jembe shambani moja kwa moja kama Nyerere. Kiongozi pekee aliyewahi kuonekana akishika nyasi shambani huku akiwa kikulima zaidi ni aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa akionekana akifanya shughuli za shambani kwa vitendo.Akizungumza na gazeti hili, mwanasheria mmoja ambaye sasa amestaafu, Dk Ngali Maita alisema Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, kwa kuzingatia uzito wa jina lake, sambamba na uzoefu wake katika uongozi, anaweza kujitengenezea au kusaidiwa kutengeneza menejimenti ya kuendesha kilimo, itakayoajiri wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), iliyojaa vijana wasomi na wazalendo.
“Inaweza kuwa hivyo kwa mzee Benjamin Mkapa, mzee Jakaya Kikwete na kwa mwingine yeyote. Ubunifu wetu katika kuwatumia marais na mawaziri
 wakuu wastaafu ni lazima uzingatie mazingira, fursa na malengo yetu.


Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda

“Tunasema wazi, hawa wastaafu walihubiri wakiwa ikulu kwamba kilimo ni uti wa mgongo nchini na rais wa kwanza (Nyerere), alianzisha Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ili kukidhi matakwa ya kauli mbiu hiyo, kwa nini leo hii tunashindwa kujipanga ‘kuwatengeneza’ marais wastaafu katika kuinua sekta ya kilimo?” alihoji msomi huyo.
Aliongeza kuwa, anatambua na kuheshimu kuwapo kwa Taasisi ya Mkapa Foundation inayohusika na masuala ya afya na kujenga nyumba za wahudumu wa tasnia hiyo, lakini pia kwa kuzingatia fursa na mazingira yetu si vibaya tukatengeneza utaratibu wa kuwa na Mkapa Agricultural Management, Mwinyi Agricultural Management na Kikwete Agricultural Management zenye kufanya kazi vijijini.
“Marais na mawaziri wakuu wastaafu wangekuwa na mchango mkubwa katika kuifanya Tanzania kujitosheleza kwa chakula kama wangekuwa nambari moja katika sekta mama ya kilimo inayoweza kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya asilimia 80,” alisema Maita.

Rais Mstaafu, Mzee Mwinyi akiendesha Power Trailler

MWALIMU NYERERE
Uchunguzi umeonesha kuwa, baada ya Mwalimu kustaafu mwaka 1985 hadi kifo chake Oktoba 14, 1999, alikuwa akijishughulisha na kilimo cha mahindi na alikuwa akiishi maisha ya kawaida kabisa kijijini wake, Butiama.
MZEE MKAPA
Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa naye uchunguzi umebaini kuwa, ana shamba lake Vigawe Bagamoyo mkoani Pwani ambalo analitumia kufugia mifugo mbalimbali lakini baada ya kustaafu, kupitia Taasisi ya Mkapa Foundation amewahi kujenga nyumba 30 za watumishi wa afya katika Wilaya za Mtwara-Vijijini, Newala na Masasi mkoani Mtwara na kuzikabidhi nyumba hizo katika hafla iliyofanyika Desemba19, 2012 kwenye Kijiji cha Imekuwa, Mtwara- Vijijini. Mzee Mwinyi, yeye ana mashamba Mkoa wa Pwani.

Rais Mstaafu Mzee Mkapa akitazama mifugo yake.

MZEE JK
Uchunguzi umebaini kwamba, mara baada ya kustaafu, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amekuwa akijishughulisha na ufugaji na kilimo cha mahindi kijijini kwake, Msoga na ana shamba la mananasi Kiwangwa, Bagamoyo.
Amekuwa akionekana kwenye vyombo vya habari mara kwa mara akiyahudumia na hata anapovuna mazao yake.

LOWASA, MALECELA, MSUYA
Waliowahi kuwa mawaziri wakuu na kuonekana wakifanya kazi mbalimbali za kilimo au ufugaji ni Edward Lowassa. Yeye, baada ya kugombea urais na kushindwa mwaka 2015 amewahi kuonekana akichunga ng’ombe katika shamba lake la Handeni mkoani Tanga.
Mzee John Malecela pia amewahi kuonekana akivuna mtama na zabibu katika shamba lake Dodoma.
Mzee Cleopa Msuya na Frederick Sumaye ni viongozi pekee wasiowahi kuonekana wakichunga au kulima kama wenzao na haijajulikana kama nao wanajishughulisha na kilimo au ufugani.
NA ELVAN STAMBULI,DAR


Facebook Blogger Plugin by

Post a Comment

 
Top