Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This


 
SIKU chache baada ya aliyekuwa mwanamuziki maarufu wa Taarab Bongo, Alhaj Mzee Yusuf kufiwa na mkewe mdogo, Chiku Khamis, mambo yamekuwa siyo shwari baada ya hivi karibuni kutinga ukweni na kudaiwa kutukanwa, kisa kikitajwa kuwa ni nguo za marehemu.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo cha kuaminika kilitiririka mbele ya Risasi Jumamosi kuwa, Mzee Yusuf alikwenda nyumbani alikokuwa akiishi na mkewe Chiku huko Chanika jijini Dar na kukusanya nguo zote za marehemu na kumpa mtu akazipeleka kwa ndugu wa mkewe huyo, Kariakoo, nyumbani kwa akina Chiku.

Chanzo hicho kilidai kuwa, ndugu walizipokea nguo hizo za marehemu ndugu yao, lakini siku chache zilizofuata Mzee Yusuf alifika nyumbani hapo kwa ajili ya kuwachukua watoto kwa ajili ya kwenda kuishi nao kwani tangu mama yao alipofariki dunia walikuwa wakiishi huko (Kariakoo).


Waombolezaji wakienda kuuzika mwili wa marehemu Chiku

WATU WAHOJI KULIKONI?
Chanzo hicho kilifunguka kwamba, kitendo cha Mzee Yusuf kutaka kuwachukua watoto hao wawili wa kike, ndipo kashikashi ilipoanza kwani mmoja wa ndugu wa Chiku alidaiwa kumporomoshea matusi Mzee Yusuf ambapo ilibaki kidogo tu kama siyo uvumilivu alitaka kuuvua ‘U-Alhaj’ ili naye aweze kujibu mapigo, jambo lililowaacha mashuhuda midomo wazi na wengine kuhoji kulikoni?
“Yaani ilikuwa ni patashika kwani Mzee Yusuf alioga matusi eti kwa kuwa tu ndugu huyo wa Chiku alikasirishwa na kitendo cha Mzee kutuma nguo haraka kabla hata ya arobaini ya ndugu yao hivyo akawa anamwambia angesubiri kwanza na siku ya kuzitoa ilikuwa lazima awepo ndugu yake mmoja asimamie maana Chiku naye inawezekana alikuwa na siri zake pia,” kilidai chanzo kilichoshuhudia sekeseke hilo.


Chiku Khamis enzi za uhai wake

RISASI JUMAMOSI MZIGONI
Risasi Jumamosi liliingia mzigoni ili kuusaka ukweli wa ishu hiyo ambapo lilianzia nyumbani kwa akina Chiku maeneo ya Kariakoo kwenye Mitaa ya Amani na Livingstone na kufanikiwa kukutana na baba wa Chiku, Mzee Khamis ambaye alitoa ushirikiano kwa kusema:
“Mimi ndiye baba mzazi wa Chiku na Mzee Yusuf alikuja kuoa hapa, lakini kuhusiana na hilo suala, siwezi kuzungumza maana mimi nina hasira sana, ngoja niwape namba za simu za dada wa Chiku ili muonane naye atawaeleza vizuri.”
NYUMBANI KWA DADA WA CHIKU
Baada ya hapo, baba huyo alitoa namba za simu za dada wa marehemu aliyemtambulisha kwa jina la Amina.

Mzee Yusuf na watoto wake.

Risasi Jumamosi lilifanikiwa kuonana na Amina nyumbani kwake Magomeni-Mapipa jijini Dar ambapo alikuwa na wanafamilia wengine akiwemo kaka yake, mama mkubwa na mdogo wake.
Amina na ndugu zake hao walisikiliza maelezo kwa makini ambapo walitaka ushahidi wa sauti ya Mzee Yusuf akikiri kutukanwa ambapo waandishi wetu walifanya jitihada za kumpata na kuzungumzia.
Baada ya kusikiliza maelezo ya Mzee Yusuf, mmoja wa ndugu hao, Amina alikuwa na haya ya kusema juu ya sakata hilo:
“Kiufupi hatuna cha kuongea kwa sasa na haina sababu ila njooni siku ya arobaini mtaujua ukweli zaidi maana familia zote mbili tutakutana pale Kariakoo nyumbani kwetu, hapo ndipo mtakapoandika habari zote mnazozitaka.”


Mzee Yusuf akiomboleza kifo cha mkewe, Chiku.

MZEE YUSUF AFUNGUKA
Mzee Yusuf alipotafutwa na kuelezwa mambo hayo yanayoendelea, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na haoni kama alikosea kwani alichokifanya hakukiuka sheria ya dini, ila wao walimuelewa tofauti na kupaniki hadi kumtukana.
“Nilifanya heshima kuwapa hivyo vitu kwa sababu kidini nilikuwa sawa na walivipokea, sipendi kuongea sana maana niliyetukanwa ni mimi na aliyenitukana ni mtu mmoja, siwezi kumtaja maana sitaki haya mambo yaendelee.
“Lakini baada ya kuwaelewesha wamekaa sawa, tuliache tu maana limeshapita, nikiongea sana nitaonekana ninatumia umaarufu wangu,” alisema Mzee Yusuf huku akiomba jambo hilo liachwe kama lilivyo.
Chiku alifariki dunia Juni 17, mwaka huu kwa matatizo ya uzazi alipokuwa akijifungua mtoto wa kiume ambaye naye hakuwa riziki katika Hospitali ya Amana jijini Dar.


Facebook Blogger Plugin by

Post a Comment

 
Top