Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail ThisKamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
Unalikumbuka lile tukio la Desemba 3 mwaka jana ambako polisi waliwakamata watoto 11 wenye umri unaokadiriwa kuwa na miaka sita hadi 14 jijini Mwanza baada ya kuizingira nyumba kwa lengo la kuwakamata watu waliowahisi kuwa majambazi?Katika tukio hilo la mwaka jana, watu watatu waliuawa na askari kukamata bunduki mbili aina ya SMG na AK47 zikiwa na magazine saba na bastola moja zote zikiwa na risasi 183.Sasa usiku wa kuamkia jana katika eneo hilohilo, polisi wamewaua watu sita wanaodaiwa kuwa ni majambazi na kukamata silaha za kivita.Waliuawa katika majibizano ya risasi ya muda mrefu na polisi katika mtaa huo wa Fumagila Mashariki, Kata ya Igoma jijini Mwanza baada ya kudhibitiwa kwenye nyumba ndogo.Diwani wa Kishili aliyeshuhudia tukio hilo, Sospeter Ndumi alisema mapambano hayo yalianza usiku wa manane hadi asubuhi kabla ya polisi kufanikiwa kuwaua watu hao na kukamata silaha mbalimbali za kivita.
Mmoja wa watu watatu waliokutwa kwenye nyumba hiyo alikimbia baada ya kuwarushia polisi bumu la mkono, kabla ya askari hao kuwadhibiti waliosalia kwa kushirikiana na wananchi.
Baada ya polisi kuondoka katika eneo hilo, wananchi waliiteketeza nyumba hiyo kwa moto.Kamanda wa Polisi Ahmed Msangi alisema jana kuwa wiki mbili au tatu zilizopita walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu ambao wanawatilia shaka kwamba wametoka Kibiti na baada ya hapo walianza kufanya upelelezi.“Tulianza kufanya upelelezi tukamkamata mtu mmoja na katika mahojiano akatuambia kundi hilo na kutuonyesha watu hao walipo wakijiandaa kufanya matukio ya uhalifu,” alisema Msangi.
“Leo (jana) saa 12 polisi walifika hapa wakiwa na huyo mtu aliyekamatwa, wakati polisi wanakaribia eneo hilo alitoa kiashiria kuwataarifu wenzake ndipo walijihami wakapiga risasi kujiandaa kukimbia, wakati wakijibizana majambazi sita walipigwa risasi wengine wawili walikimbia,” alisema.
Alisema katika tukio hilo wamekamata silaha SMG na AK 47, magazini mbili kila moja ikiwa na risasi 30, risasi 36 za AK 47 ambazo zilikuwa nje magazine, risasi moja aina ya rafal, risasi nane za shotgun na ganda moja la shortgun
Alizitaja silaha nyingine kuwa ni bastola nne za kienyeji, sare za jeshi la nchi jirani, kofia sita za kuziba uso, kitambaa cha kichwani, nusu kanzu, nguo mbalimbali za kiume, mabegi matatu yaliyokuwa yakihifadhi silaha hizo, dagaa, unga baiskeli mbili na pikipiki moja.
Kamanda Msangi alisema bado kuna viashiria vya uhalifu lakini jeshi hilo linaendelea na operesheni ya kuwasaka wahalifu akiwataka wananchi kuondoa hofu akisema hakauna atakayesalimika.Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliwataka viongozi wote wa mtaa na wenyeviti kuwa na leja ya wakazi wanaoishi katika mtaa husika huku wakiwa na taarifa za wageni wote wanaoingia na kutoka kwenye mitaa yao.
Kadhalika, Mongella aliagiza kuanzishwa na kuimarishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama kwenye mitaa yote na kusema atafanya ukaguzi wa kushtukiza na ambao atakuta wameshindwa kutimiza jukumu hilo, watakuwa wamejiondoa kwenye nafasi zao.
“Nikija hapa nikakuta hamjaweka ulinzi shirikishi mtaona, toeni taarifa nami nitakuwa nakuja huku kwa kushtukiza nikija hapa nikakuta hamajaweka ulinzi na kutoa mwanya kwa watu wanaowadhulumu wenzao mtakiona cha moto,” alisema Mongella.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama endapo watamhisi mtu vibaya.
“Hata kama ukimhisi mtu vibaya toeni taarifa, wenye utaalamu watathibitisha.”


Facebook Blogger Plugin by

Post a Comment

 
Top