Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema wakati kikisubiri ombi la IGP Said Mwema kukutana tena na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, wanaipeleka hoja yao ya kuwawajibisha Waziri wa Elimu Dk. Shukuru Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo bungeni.
Kauli ya CHADEMA ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
CHADEMA iliahirisha kwa muda maandamano yake ya kuwashinikiza viongozi hao kujiuzulu kutokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, yaliyokuwa yafanyike katika majiji manne ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Arusha.
Hatua hiyo ilikuja baada ya IGP Mwema kuzungumza na Mbowe na kuwaomba wayasitishe kwa muda ili kupisha ziara ya Rais wa China, Xi Jinping aliyeitembelea Tanzania kuanzia Machi 24.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo alisema mkutano wa Bunge unatarajiwa kuanza Aprili 9, na hivyo wataanza kuchukua hatua kadhaa za kibunge wakati wakiendelea kuvuta subira kujua kitakachojiri katika mazungumzo ya viongozi hao.
“Lengo ni kumbana Waziri Mkuu Mizengo Pinda atoe taarifa bungeni alitekeleza vipi mapendekezo ya siku za nyuma,” alisema.
Alisema kuwa azma ya maandamano ipo pale pale na kwamba Waziri Mkuu naye ni mtuhumiwa kwa vile sera zote za elimu, mamlaka ya utekelezaji wa sera hizo ni ofisi yake.

“Tutaenda bungeni, wakitumia vibaya kanuni za Bunge sisi tutarudi kwa wananchi kwani kwa mujibu wa katiba yetu iliyopo, hata kama ni mbovu, ibara ya nane inasema kuwa wananchi ndio waamuzi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mnyika alisema kuwa wamesikitishwa na kauli ya CCM kudai CHADEMA wametumwa na mafisadi kutaja miradi iliyoingiwa kinyemela baina yao na Wizara ya Uchukuzi kuhusu upanuzi wa bandari kavu jijini Dar es Salaam.
Alisema ingefaa CCM wawaeleze mafisadi ni akina nani kwani CHADEMA ilishawataja Mwembeyanga wakatishia kwenda mahakamani, lakini wakashindwa kufanya hivyo.
“Wajitokeze waseme akina nani ni mafisadi wanaotaka kwenda Ikulu kwa njia zozote ikiwemo kututumia sisi,” alisema.
Mnyika aliongeza kuwa CHADEMA imefurahishwa na hatua ya CCM kukiri kumiliki Kampuni ya Jitegemee Trading na kujitolea haraka kujibu kuwa hatua za sasa zilikuwa ni barua za makubaliano wala si mikataba na Wizara ya Uchukuzi.


Facebook Blogger Plugin by

Post a Comment

 
Top