Pages

Labels

Monday, June 4, 2012

Benki ya CBA kuwanufaisha wateja wake 
BENKI ya Commercial of Africa Tanzania Limited imeanzisha promosheni ambapo wateja wake watanufaika na zawadi mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha wateja binafsi wa Benki hiyo, William Mungai alisema promosheni hiyo itasaidia kuboresha maisha ya wateja wao na wafanyakazi wa benki hiyo.
Alisema promosheni hiyo kwa mwezi itahusisha makampuni, wateja binafsi ambapo mteja atatakiwa kufungua akaunti mpya kwa kiwango cha chini cha milioni 50 ataingia kwenye droo ya kujishindia Laptop.
Alisema mteja akiweka pesa marambili zaidi kwenye akaunti yake ya Current kwa kiasi kisichopungua milioni 20 naye ataingia kujishindia Laptop.
"Mteja atakaye mshawishi mshirika wake mfanyabiashara, SME, Msambaji, rafiki kufungua akaunti kwa kiasi kisichopungua milioni 15 ataingia kwenye droo ya kujishindia kompyuta ya mezani''. alisema Mungai.
Aliongeza kuwa watu wote watakaokidhi vigezo cha kwanza na cha tatu wataingia kwenye droo kubwa ya kushinda kompyuta na printa.
Alisema kwa wateja binafsi wanapaswa kufungua akaunti mpya kwa kiwango cha chini cha milioni 1 na kuiongia kwenye droo ya kujishindia Tv ya Plasma.
Alisema mteja akiweka fedha zaidi ya mara mbili katika akaunti yake kwa kiasi kisichopungua sh. milioni 500 ataingia kwenye droo ya kujishindia DVD Home Theater.
Alisema kwa mtu atakaye mshawishi rafiki, mshirika na kufungua akaunti ya familia yaani mke na mtoto mmoja kwa kiasi kisichopungua sh. milioni 1 ataingia kwenye droo ya kujishindia TV ya Plasma.
Alisema kwa wateja watakaoingia robo mwaka ambapo itakuwa ni mwisho wa kampeni na kukithi vigezo namba moja na tatu wataingia kwenye droo kubwa ya kushinda Friji, DVD Home Theater na TV Plasma.
Alitoa mwito kwa waqnanchi kufungua akaunti mpya, kuweka fedha mara mbili au kumshawishi mtu au kampuni kufungua akaunti ili kushinda zawadi hizo.

Wanakibasila wapinga fidia ya mabasi yaendayo kasi DART
WAKAZI wa Kibasila Kata ya Gerezani ambao nyumba zao zilibomolewa kupisha ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo kasi wamepinga fidia inayotolewa na DART wakidai inapingana na sheria.
Akizungumza katika mkutano na wananchi hao Dar es Salaam juzi, Wakili  Dk. Edmund Mvungi kutoka Shirika la Wanasheria wa South Law Chambers alisema malipo hayo ni batili.
Alisema DART kwa siku kadhaa mfululizo imekuwa ikitoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuwa waliobomolewa waende kuchukua fedha za fidia.
Alisema DART walidai kuwa wakazi hao waliobomolewa nyumba hizo watalipwa donge nono la fidia ya sh.milioni 30 kufidia ardhi yao iliyotwaliwa na serikali.
Alisema sheria haielekezi hivyo fidia ya ardhi hutolewa baada ya bomoabomoa kwani fidia ni matokeo ya makubaliano kati ya serikali na wamiliki halali wa ardhi inayochukuliwa na kuwa sheria inaagiza kuwa kigezo ni bei ya soko.
Amesema DART kwa makusudi wameamua kukiuka sheria kwa kuanza kutangaza kufanyika kwa malipo hayo licha ya jambo hilo kuwa mahakamani.
Alisema fidia hiyo ni kinyume na sheria hivyo wao wamependekeza kila mmoja wao kulipwa sh. bilioni 2 kama fidia ardhi yao na usumbufu wa kubomolewa makazi yao.
Alidai wanakusudia kufungua kesi   mahakamani dhidi ya Mkurugenzi wa DART Kosmas Tekule kwa kukikuka sheria kwa kuanza kuwarubuni baadhi ya wananchi hao na kuanza kulipa fidia wakati suala hilo lipo mahakamani.
Katika hatua nyingine alisema wanakibasila hao hawawatambui wenzao 28 ambao wamerubuniwa kuchua fidia hiyo na kupitia kamati yao bandia ambapo walidai uongozi wanaoutambua ni ule unaosimamia kesi yao namba 44.
Viongozi hao wanaotambulika wametajwa kuwa ni Abdalla Mkongo, Jumbe Lilla, Hussein Batenga na Athman Kiwaga.
Alisema matangazo yanayotolewa na DART ni uchochezi na uvunjaji wa sheria kwani anayetoa matangazo hayo anaingilia kesi iliyopo mahakamani.

KUENGULIWA KWA MAJINA YA WATU WANAOKUBALIKA KULIIGHARIMU CCM UCHAGUZI WA 2010


Katibu wa CCM Kata ya Tunduma Hemed Steven
 

 
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Tunduma wilayani Momba mkoani Mbeya kimesema kuwa kuanguka kwa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ulichangiwa na viongozi wa Wilaya kuengua majina ya wagombea waliochaguliwa kwa kura nyingi na wanachama kuwania nafasi za Udiwani na Ubunge.
Akizungumza katika kikao kilichoitishwa na Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), mjini humo Katibu wa CCM Kata ya Tunduma Hemed Steven alisema kuwa chama hakipaswi kujilaumu kwa nini kilianguka katika uchaguzi huo bali kinapaswa kujilaumu kwa nini kilisimamisha wagombea wasiochagulika.
Alisema kuwa CCM inaangushwa na viongozi wa juu ambapo mara wanapopelekewa majina ya wagombea huyaengua kwa maslahi zao na hivyo kusababisha wananchi kuamua kupiga kura za chuki na kuwaangusha wagombea waliosimamishwa kwa maslahi ya viongozi.
‘’Tunaomba tuwaeleze viongozi wa juu ngazi za wilaya, majina yaliyochaguliwa na wanachama yasienguliwe, sisi tumewaamini kuwa wana vigezo mnapobadilisha majina tuliyoyapendekeza msitafute mchawi,’’alisema Steven.
Alisema watendaji wabovu ndani ya chama hicho ndio wanaosababisha chama hicho kishindwe kufanya vizuri na kutekeleza ahadi na ilani za chama ipasavyo hivyo ni wakati muafaka kwa viongozi ambao wanaona hawakidhi mahitaji kujiengua mapema.
''Tunawapa siku 14 watendaji msiowajibika katika chama, hatuoni kazi kuwafukuza uanachama kama mnakwamisha maendeleo ya chama na wananchi, hizi ndio dalili zinazosababisha tushindwe katika uchaguzi na wananchi wartukatae,''alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM kata ya Tunduma Danny Mwashiuya alisema kuwa kukosekana kwa watu makini wa kukisema chama kinapokosea ndio sababu nafasi hiyo ya kukisema chama inachukuliwa na upinzani na kutumia kama kigezo cha ushindi katika uchaguzi.
''Tunapokosea tusemane wenyewe kwa wenyewe humu humu...tunawaachia mwanya wapinzani watuseme majukwaani, hili ndilo linalotuangamiza,''alisema Mwashiuya.
Naye Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Mbozi Agusta Ndunguru alisema kuwa dhamana ya uongozi wa CCM uko mikononi mwa wanachama wenyewe na kwamba tatizo la kukosekana kwa ushirikiano baina ya viongozi na wanachama ndio sababu ya chama hicho kushindwa katika chaguzi mbalimbali zinazoendelea.
Ndunguru alisema migogoro inayokitafuna chama cha Mapinduzi inasababisha kuibuka kwa makundi ambayo mwishowe huibua dhana kukichukia chama na kuzalisha makundi ya watu wanaokihama chama hicho.

WARATIBU WA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2012 WATAKIWA KUSIMAMIA FEDHA NA RASIRIMALI ZINAZOTOLEWA


Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Sensa, Dk. Albina Chuwa akisisitiza jambo.
 
.Ikiwa imebaki miezi michache kabla ya kuanza kwa zoezi la Sensa ya watu na makazi nchini  serikali imewataka waratibu wa zoezi hilo  kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu fedha na rasilimali zinazopelekwa kwenye mikoa na wilaya zote nchini ili kufanikisha zoezi hilo.
 
Akizungumza na waratibu wa Sensa  ya watu na makazi 2012 kutoka  katika  mikoa na wilaya zote nchini  leo mjini Morogoro naibu katibu mkuu Ofisi ya Waziri mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw.Alphayo Kidata amesema kuwa zoezi hilo litafanikiwa kwa  kiwango kikubwa kama waratibu  hao watasimamia ipasavyo matumizi  ya fedha na rasilimali zinazopelekwa  katika meneo yao. 
 
Amesema  jukumu la usimamizi wa Sensa kwenye ngazi ya mikoa na wilaya ni la viongozi wa maeneo hayo na kufafanua kuwa kushindwa kwa zozei hilo katika wilaya au mikoa husika ni kiashirio cha viongozi hao kushindwa kusimamia majukumu yao kwani takwimu zitakazopatikana zitatumiwa pia na mamlaka za mikoa na wilaya katika shughuli za maendeleo.
 
"Napenda kusisitiza kuwa mafanikio ya Sensa ya watu na makazi 2012 yanawahusisha pia viongozi wa mikoa na wilaya zote nchini hivyo usimamizi usioridhisha kwenye mikoa na wilaya zetu utasababisha upatikanaji wa takwimu zisizosahihi na hivyo kuathiri maendeleo ya maeneo hayo hivyo tunawajibu wa kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa" amesisitiza. 
 
Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa zoezi hilo serikali imeiweka Sensa ya watu na makazi kuwa moja ya vipaumbele vyake kwa mwaka huu na kuongeza kuwa zoezi hilo ambalo ni la kitaifa licha ya kuwa jukumula kila mtanzania  waratibu hao wana wajibu wa kusimamia ufanikishaji wa zoezi hilo.
 
" Zoezi la ukusanyaji wa takwimu katika zoezi la Sensa haliwezi kutimizwa iwapo kazi ya ukusanyaji wa takwimu katika maeneo yote ya wilaya na mikoa hamtaifanya kwa umakini na jukumu lenu kuhakikisha kuwa mnatekeleza maagizo yote kutoka ngazi za juu ili kufanikisha zoezi hilo" amesema Bw. Kidata.
 
Amewataka waratibu hao kuwa wasimamizi wazuri na kuhakikisha kuwa uteuzi wa makarani na wasimamizi wa zoezi la sensa unafanywa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa ili kuondoa manung'uniko na kuleta ufanisi wa kazi wa kazi wakati wa zoezi hilo.
 
Amefafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar ndio waratibu wa Zoezi hilo na Kufafanuz kuwa sensa ya watu na makazi kwa mwaka huu inalenga kupata takwimu sahihi ambazo zitasaidia kutunga  Sera  na kupanga programu za maendeleo za kuiwezesha serikali kupanga na kutathmini mipango ya maendeleo nchini.
 
Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu  Bw. Ephraim Kwesigabo  amesema kuwa hivi sasa maandalizi yamekamilika na kuongeza kuwa mafunzo hayo ya awali kwa waratibu wa Sensa kutoka mikoa na wilaya zote nchini yanalenga kuwajengea uwezo waratibu hao ili waweze kusimamia vyema maeneo yao wakati wa zoezi la Sensa.
 
Amesema mafunzo hayo yanajadiliwa na kutoa ufafanuzi  wa masuala mbalimbali ya ufanikishaji wa zoezi hilo yakiwemo namna ya kuwapata makarani na wasimamizi wa Sensa, maandalizi ya mafunzo katika wilaya  na mikoa yao, usimamizi wa zoezi la kuhesabu watu na ubora.
 
Naye Mratibu wa taifa wa Sensa ya watu na makazi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Irenius Ruyobya amefafanua kuwa tayari maandalizi ya ufanikishaji wa zoezi la sensa ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi hilo yamekwishafanyika.
 
Pia amefafanua kwa zoezi la  uchapaji wa karatasi za maswali ya sensa (madodoso) linaendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa  huku akifafanua kuwa zoezi hilo litafanyika mwezi Agositi tarehe 26 kama ilivyopangwa na kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa watakaopita katika maeneo yao kwa lengo la kukusanya takwimu.

H. BABA APAGAWISHA TAMASHA LA TIGO MBULU


Msanii wa muziki  wa kizazi kipya Bongofleva H. Baba akiwapagawisha mashabiki kwenye Tamasha laTigo lilofanyika katika wilaya Mbulu katika tamasha hilo kila mteja wa tigo aliweza kujinyakulia zawadi  mbalimbali kutoka tigo.
Baadhi ya wateja wa tigo wakipata huduma kutoka kwa watoa huduma wa kmpuni hiyo wakati wa Tamasha hilo,

Ripoti yasema Rwanda inaunga uasi DRC


Ushahidi mpya unaonyesha kwamba jeshi la Rwanda linawasaidia waasi katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch.Shirika hilo limesema waasi wa zamani wameelezea jinsi Rwanda iliwasajili wapiganaji kujiunga na waasi pamoja na kutoa silaha.
Rwanda pia imedaiwa kutoa hifadhi kwa Jenerali muasi Bosco Ntaganda,anayetakikana na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC. Serikali ya Rwanda imekanusa kuwafadhili waasi hao.
Waandishi wa habari wamesema japo ripoti hii haijailaumu moja kwa moja serikali ya Rwanda kwa kuwafadhili waasi, hata hivyo imeutaka utawala wa Kigali kuhakikisha vitendo vya kuwasajili wapiganaji na kuvukisha silaha vinadhibitiwa.
Maasi yanayoendelea Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanaongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye zamani alikuwa kamanda katika kundi la waasi wa CNDP lakini baadaye lilijumuishwa katika jeshi la Congo mwaka 2009 kufuatia mkataba wa amani

Chelsea yakamilisha mipango ya Hazard


Klabu ya soka ya England ya Chelsea imetangaza katika tovuti yake kwamba hatimaye imekubaliana na klabu ya Lille ya Ufaransa kwamba mchezaji wa kimataifa ya Ubelgiji, Eden Hazard, atajiunga na klabu hiyo ya Stamford Bridge msimu ujao. Mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 21, tayari afya yake imekaguliwa na klabu ya Chelsea, na imeonekana hana tatizo lolote.
Walipochukua ubingwa wa ligi ya klabu bingwa, nilijiuliza, "Kwa nini sio Chelsea?", alisema Hazard.
"Kulikuwa na mvutano kati ya Chelsea na Manchester united, lakini binafsi naona Chelsea ndio mradi bora zaidi. Ni klabu cha ajabu."
Inaarifiwa kwamba Chelsea wameamua kutoa pauni milioni 32 kumpata kijana huyo, na ambaye akizungumza na kituo cha redio cha nchini Ufaransa, RMC, aliongezea: "Chelsea ni timu changa, na nitakuwa na nafasi bora zaidi ya kucheza."
"Ikiwa nitajitahidi kucheza vyema nikiwa Chelsea, huenda nikapata nafasi katika timu."
Hazard alikuwepo katika kikosi kilichoshinda ligi wakati Lille ilipopata ubingwa mwaka 2010-11 na katika msimu wake wa mwisho, alifanikiwa kufunga magoli 21 katika mechi 48.
Katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Nancy mwezi uliopita, alifanikiwa kupata hat-trick (magoli matatu) wakati timu yake ilipocheza dhidi ya Nancy.
Lakini alishindwa kuvuma wakati Ubelgiji iliposhindwa na England katika mechi ya kirafiki Jumamosi iliyopita.
Hiyo ilikuwa ni mara yake ya 28 kuichezea timu yake ya taifa ya Ubelgiji.
Hazard sasa ni mchezaji wa pili kusajiliwa Chelsea tangu dirisha la usajili la mwezi Januari, wa kwanza akiwa ni mchezaji wa kimataifa wa Ujerumani, Marko Marinas.

Murray amshinda Gasquet


Andy Murray, mchezaji bora zaidi wa kiume katika mchezo wa tennis nchini Uingereza, amefanikiwa kuingia robo fainali, baada ya kumshinda Richard Gasquet wa Ufaransa katika mashindano ya French Open, uwanja wa Roland Garros.
Murray, ambaye amepangwa kama mchezaji wa nne bora zaidi katika orodha ya wachezaji mahiri katika mashindano hayo ya Ufaransa, alilemewa katika seti ya kwanza, na inaelekea maumivu ambayo yalikuwa yanamharibia mapambano yake ya awali yalikuwa yamembana tena.
Hata hivyo aliweza kujikakamua na kupata ushindi katika seti ya pili, kabla ya kumuondoa Gasquet kwa 1-6 6-4 6-1 6-2.
Murray sasa Jumatano atapambana na David Ferrer wa Uhispania katika kujitahidi kuingia nusu fainal

ECOBANK YAZINDUA PROMOSHENI YA SHINDA BABKUBWA NA ECOBANK LEO JIJINI DAR ES SALAAM


Mkurugunenzi maendeleo Ecobank katikati Bw;Samwel Ayim akiongea na waandishi wa habari leo makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa promosheni ya shinda Babkubwa na Ecobank  Bw;Samwel Ayim  amesema gari ambalo litashindaniwa ni aina ya Hyundai ix35 kushoto ni mkuu wa kitengo cha Huduma kwa wateja Bi Joyce Mlai, na kulia Head corporate Bw. Linley Kapya.
Waandishi wa habari wakiwa katika uzinduzi huo wakifuatilia kwa makini yaliojiri kwenye mkutano huo
Bw;Linley Kapya katikati akionyesha gari ambalo litashindaniwa katika promosheni hiyo

MANJI AJICHUKULIA FOMU YA KUGOMBEA UENYEKITI, AMCHUKULIA NA BEN KLEB YA UMAKAMU MWENYEKITI


Hayawi hayawi sasa yamekuwa!!!!!
Taarifa rasmi na za uhakika nilizozipata kutoka makao makuu ya klabu ya Dar Young Africans ni kwamba mwanachama maarufu na tajiri wa klabu hiyo, mfanyabiashara Yusuph Mehebob Manji amechukua fomu za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa klabu ya Yanga.

Manji ambaye kwa muda mrefu sasa amekuwa akiisadia Yanga kiuchumi zaidi, nusu saa iliyopita ameenda kwenye makao makuu ya klabu hiyo na kuchukua fomu za uenyekiti bila kuweka wazi kama kwa ajili yake au amemchukulia mtu kwa ajili kugombea nafasi hiyo.

Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na taarifa juu ya Manji kutaka kugombea nafasi hiyo japo mwenyewe bado hajathibitisha, ingawa kitendo chake cha leo kimezidi kuupa nguvu uvumi wa kwamba anataka kugombea nafasi ya kuwa bosi wa Yanga.

Wakati huo huo taarifa nyingine zinasema kuwa aliyekuwa mjumbe Kamati ya Mashindano ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb naye muda wowote kutoka sasa atadondoka makao ya Yanga kwa ajili ya kuchukua fomu za kugombea umakamu mwenyekiti.

Mwanachama mwingine maarufu wa klabu hiyo Issac Mazwile naye ameshachukua fomu za kugombea nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji.


Yusuph Manji

Muda mchache uliopita nilitoa taarifa za kuhusu Yusuph Manji kuchukua fomu za kugombea uenyekiti wa klabu ya Yanga, bila kuwepo kwa uthibitisho kwamba amechukua kwa ajili yake au kamchukulia mtu.
Ben Kleb akimkabidhi jezi Haruna Niyonzima
Lakini sasa kwa taarifa nilizozipata kutoka kwa mmoja ya wajumbe wa kamati ya uchaguzi wa Yanga, amethibiisha kwamba Manji amejichukulia fomu mwenyewe ya kugombea uenyekiti, huku akimchukulia aliyekuwa mjumbe wa kamati ya usajili Abdallah Ahmed Bin Kleb fomu za kugombea umakamu mwenyekiti.

Mbunge Kukamatwa Kwa Rushwa:Kauli Ya KafulilaTAMKO LA NDUGU DAVID KAFULILA KUHUSU MBUNGE WA JIMBO LA BAHI KUKAMATWA NA TAKUKURU KWA RUSHWA.
JUNE 03, 2012
Kwanza niwashukuru ndugu zangu wanahabari kwa kuitikia wito wangu kukubali kuja kunisikiliza. Mtakuwa mmesikia na kusoma kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuhusu taarifa ya aibu inayolikumba Bunge letu tukufu kufuatia taarifa kutoka vyombo vya dola kuwa mbunge mwenzetu kutoka jimbo la Bahi Ndugu Omary Badwel anashikiliwa na vyombo vya dola kwa kosa la jinai na la aibu sana la rushwa.

Ningependa kuwakumbusha wana habari kuwa nimepata kuzungumza Bungeni mwaka jana 2011 kuhusu tabia ovu kwa baadhi ya wabunge kuomba rushwa watumishi wa serikali katika mchakato wa kusimamia serikali. Ilikuwa ni Bunge la mwezi June, tarehe 13, 2011 wakati nikichangia hoja ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Hapa nilitoa taarifa iliyowahusu wabunge watatu akiwemo huyu anayeshikiliwa na vyombo vya dola sasa, Ndugu Omary Badwel. Kwakuwa hakuna hatua iliyochukuliwa, leo napenda niweke msimamo wangu wazi katika maeneo yafuatayo;

1. Kwakuwa nilijitahidi sana kwa kila namna kujenga heshima ya kamati hii ya LAAC bila kupewa ushirikiano toka kwa wadau wote, TAMISEMI pamoja na BUNGE, naomba kutamka rasmi kuwa sina imani tena na Kamati hii kwakuwa imepoteza uhalali kuweza kuendelea kuwa kamati ya kusimamia na kudhibiti hesabu za serikali.

2. Kwa kuzingatia hoja hiyo, Ni wajibu wa Spika kutafakari upya kuhusu hadhi ya Kamati hii na kuipanga upya kwa maslahi ya Umma, heshima na hadhi ya Bunge letu.

3. Nikiwa mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Bunge, Na kwakuwa linayo mamlaka ya kumvua ubunge mbunge yeyote kwa azimio la Bunge, nitaiomba Kamati kushughulikia suala hili kibunge na kuhakikisha tunakwenda na azimio katika mkutano ujao wa Bunge kuhakikisha hatua stahiki zinachulikuwa kulinda heshima ya Bunge ili muhusika aendelee kuchukuliwa hatua za kijinai kama raia wa kawaida.

4. Kwakuwa suala hili linahusu heshima na hadhi ya Bunge, Ni muhimu Kamati ya Uongozi kuhakikisha suala hili linakuwa la kwanza katika ratiba za vikao vya mkutano ujao. Napenda kurudia kuwa, nilisema mwanzo na hakuna aliyechukua hatua. Hii ni mara ya mwisho na ninaahidi kutoendelea kushiriki tena vikao vya kamati hii ya aibu kama Mh. Spika hataona busara na umuhimu wa kuipangua kamati hii. Serikali legelege ni matokeo ya Bunge legelege kwakuwa ni kazi ya Bunge kusimamia na kuidhibiti serikali kikatiba. Watendaji wa serikali kujua bei za wabunge ni msiba.
………………………………………… 
David Kafulila (MB).

MBUNGE WA BAHI OMARY BADWEL, AFIKISHWA KIZIMBANI LEO KWA KESI YA KUDAI RUSHWA


 Mbunge wa  Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel, akiwa chini ya ulinzi wakati alipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo kwa ajili ya kusikiliza kesi inayomkabili. Mbunge huyo alikamatwa jana kwa kile kilichodaiwa kudai na kutaka kupokea Rushwa baada ya kukamilika kwa mitego ya Wana TAKUKURU katika Hoteli ya Peacock iliyopo maeneo ya Mnazi Mmoja jana. 
 Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel, akiwa chini ya ulinzi wa Polisi wakati akitoka Mahakamani huku baada ya kusomewa mashitaka mawili ya rushwa ya sh. milioni 1, aliyokuwa akiitaka kutoka kwa  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana.
Wakili wa Mbunge wa Bahi, Omary Ahmed Badwel, Mpare Mpoki (kushoto) akitoka Mahakamani.

Na Mwandishi Wetu, Jijini
MBUNGE wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel (43) leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kosa la rushwa ya shilingi Milioni moja toka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana.
Wakili wa Takukuru, Janeth Machullia na Ben Lincoln, walidai mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba, kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ya rushwa. 
Wakili Machullia, alidai kuwa kosa la kwanza ni la rushwa kinyume na kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007, kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam , Badwel, akiwa ni Mbunge wa Bahi na Mjumbe Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na wakati huo akiwa ni ofisa wa serikali kwa maana ya sheria ya Takukuru, alitenda kosa la kushawishi ili apewe rushwa ya jumla ya Shilingi milioni nane kutoka kwa, Sipora Liana, ili kiasi hicho cha fedha aweze kuwapelekea wajumbe wenzake wa Kamati hiyo ya Bunge ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya mwaka 2011/2012 ya Halmashauri hiyo.
 Wakili Machullia, alidai shitaka la pili ni kwamba kati ya Juni 2 mwaka huu, katika Hoteli ya Peacock, mshitakiwa akiwa na nyadhifa zake zote hizo alipokea rushwa ya Milioni moja kutoka kwa Liana ili aweze kwenda kuwashawishi wajumbe wa Kamati hiyo ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya Halmashauri ya Mkuranga huku akijua kufanya hivyo ni kosa.
 Hata hivyo mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki, alikanusha mashitaka yote na wakili wa Machullia, alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Kahamba, alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao kila mmoja atasaini bondi ya shilingi milioni nne na kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani, sharti ambalo lilitimizwa na mshitakiwa huyo na akapata dhamana. 
Hakimu Kahamba, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuja kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo

ASHA BARAKA ATAMBULISHA UONGOZI MPYA TWANGA PEPETAMkurugenzi wa African Stars Entertainment (ASET), akitambulisha safu mpya ya uongozi wa bendi. Muddy Pizzaro anakuwa Msemaji wa bendi, Muddy K anakuwa Meneja Matukio, Omary Baraka anaendelea kuwa |Mkurugwenzi Mtendaji, Amigolas anakuwa Meneja wa Bendi, Luiza Mbutu anaendelea kuwa kiongozi wa bendi, akisaidiwa na Saleh Kupaza. Kiongozi wa wanenguaji anaendelea kuwa Maria Salome kwa wanawake na kwa wanaume anaendelea kuwa Sidy  Boy. Shughuli hii imefanyika katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, asubuhi hii.

Asha akiwa amezungukwa na Waandishi
Asha akizungumza na Waandishi 

Amhela Msangi wa TBC kushoto akipata kitu cha supu

Waandishi wakimsikiliza kwa makini Asha

Victor wa Spoti Starehe kulia na Kambi Mbwana wa Mtanzania

Shakour wa Global na Mateja kulia

Meza kuu, wanamuziki nas viongozi

Wanenguaji wa bendi

Mkurugenzi Mtendaji, Omary Baraka kazini

Luiza na Asha

Mabosi wapya; Muddy Pizzaro kushoto na Muddy K kulia.

NCCR-Mageuzi Acheni Kupiga Mayowe, Acheni Umma Uone Wenyewe!

Ndugu zangu, 

NCCR- Mageuzi wamewajia juu wapinzani wenzao, Chadema. Wanawashutumu Chadema kwa kuwaita NCCR- Mageuzi  ' CCM 'B'! 

Tumemsikia Mbunge Machali akionyesha machachali yake ya kisiasa. Naye amewaita Chadema ' mahayawani'  Neno ' hayawani' lina maana ya ' mnyama'- mtu kuitwa hayawani ina maana ya mtu ' mshenzi'- usiyestaaribika kama alivyo mnyama. Nalo ni tusi, si ajabu nao Chadema wakaja na kauli ya kuwataka NCCR- Mageuzi wawaombe radhi kwa kuwatukana hadharani!

Lakini tuanze na aliyeanza;  Machali wa NCCR- Mageuzi  anasema; Chadema, ama wawaombe radhi hadharani vinginevyo NCCR - Mageuzi inaweza kuwapeleka mahakamani. Ndio, kiduku cha kisiasa kimechanganya . Naam, siasa ni burudani pia.

 Nionavyo, NCCR- Mageuzi hawana sababu ya kutoka na kupiga mayowe hadharani. Walichopaswa ni kufanya kinyume chake, kuwaimbia wenzao; " Chadema , acheni kupiga mayowe, acha umma uone wenyewe!"

Ni kazi ya NCCR- Mageuzi sasa kuonyesha umma kuwa wao si ' CCM 'B''- Full stopp! Tumemwona David Kafulila leo magazetini - Kafulila kapambana vikali kuishutumu kamati ya Maadili ya Bunge juu ya sakata la mbunge wa CCM kupokea rushwa ya milioni moja. Ametishia kujitoa kwenye kamati hiyo.

Na jana kwenye runinga Kafulila kasema, ili kulinda heshima ya Bunge,  itungwe sheria kwa mbunge anayepokea rushwa na kufikishwa mahakamani avuliwe ubunge na aende mahakamani kama raia wa kawaida. 

Ndio, Kafulila ameonyesha, kuwa kama kuna wanaodhani NCCR- Mageuzi ni CCM' B', basi yeye hayumo kwenye timu hiyo. Wengine ndani ya NCCR- Mageuzi wafuate nyayo za Kafulila.

Chama cha upinzani kionyeshe wazi kuwa ni chama cha upinzani na si cha upinzani kwa wapinzani wenzake. Hilo la mwisho hata kama kisipoitwa ' CCM 'B' na wapinzani wenzake, kijue, kuwa Watanzania wa leo si wa jana. Wanatembea na ' mihuri' yao mifukoni.  Wanatafakari kauli na misimamo ya wanasiasa na vyama vya siasa , kisha wanagonga 'mihuri' yao- kimyakimya wakisubiri 2015. 

Naam, NCCR- Mageuzi kina uzoefu wa miaka mingi kwenye siasa za upinzani.  Ichunge sasa, isije NCCR- Mageuzi ikawa NCCR- Manung'uniko! Hili la kuitwa ' CCM B' na Mbunge Wenje wa Chadema ni issue ndogo kisiasa .

 Kwa NCCR- Mageuzi kuikuza vile kumezidi kuwafanya wapiga kura wahisi ina ukweli ndani yake. Maana, kwa  wanasiasa na vyama kukebehiana majukwaani ni jambo la kawaida.

Kwenye uchaguzi uliopita tumesikia hata wapinzani wakiitwa ' fotokopi' ya CCM! Hakuna hata mpinzani mmoja aliyeonekana kwenye ofisi ya wakili  kutaka kufungua mashtaka ya kudharauliwa kwa kuitwa ' fotokopi'.

 Si tunaona leo, huyo aliyetamka wapinzani ni ' fotokopi' anakaa na kunywa chai na hao ' fotokopi' huku wakizungumza masuala ya Katiba!

Afrika 'origino' inaweza kuanzia na 'fotokopi'! Mwanasiasa usikonde kwa kuitwa ' fotokopi'.  CCM 'B' yaweza kuwa na maana ya ' fotokopi' ya ' A'.  Na katika siasa ' A' inaweza kuwa ' fotokopi' ya 'B'. Ni kujua tu namna ya kuchanga karata za kisiasa.

Ndio maana ya kusema, siasa ni burudani pia. Na kuna mwanasiasa ambaye anapaswa kupigiwa mfano. Mimi namkubali sana Nape Nnauye. Huyu jamaa hata atukanwe vipi. Atajikung'uta na kurudi tena kupambana jukwaani.  Humsikii Nape  kuzungumzia lugha ya kuwafikisha mahakamani wanaomkebehi yeye binafsi au chama chake.

Na jana Nape akiwa Songea kanifanya nicheke  sana alipowaita wana- CCM wenzake wanaokwenda upinzani kuwa ni  ' Oil chafu!' Sisi tunaoendesha  magari mabovu mabovu tunajua haswa maana ya ' Oil chafu'.

Na katika hilo Nape anatuambia kuwa CCM inapopoteza wanachama wake ni sawa na chama hicho ' kumwaga Oil chafu'. 

Na je, wanachama hao hao , wanapobadilika tena na kurudisha kadi za Chadema na kujiunga na CCM ina maana  ni ' Oil chafu' iliyojisafisha yenyewe au kusafishwa na Chadema?!

Haki ya Mungu, siasa ni burudani pia!

Ajali ya ndege yawaua zaidi ya watu 150


Siku tatu za maombolezi ya kitaifa zimetangazwa kuanzia leo nchini Nigeria kufuatia ajali ya ndege ambapo zaidi ya 150 walikufa.
Ndege hiyo aina ya Boeing MD-83 iliangukia eneo moja la kuchapisha karatasi na makaazi mjini Lagos kabla ya kulipuka. Makundi ya wokozi yamekuwa eneo la ajali usiku kucha.
Ndege hiyo inamilikiwa na kampuni ya Dana Air ambayo hutoa huduma zake kati ya mji wa Abuja na Lagos. Ajali hiyo ilitokea katika mji wa Iju Kaskazini mwa uwanja wa ndege.Taarifa zinasema abiria wote katika ndege hiyo walikufa. Hakuna majeruhi katika eneo la ajali japo haijabainika rasmi ni watu wangapi ambao wamekufa.
Rais Goodluck Jonathan ameamrisha kufanyika uchunguzi kamili kubainisha kilichosababisha ajali hiyo.
Mwandishi wa BBC Mjini Lagos Will Ross amesema hapo mwezi Mei ndege nyingine inayomilikiwa na kampuni ya Dana Air ilipata hitilafu za mitambo na kulazimika kutua ghafla.
Nigeria kama nchi nyingi Barani Afrika inakumbwa na matatizo ya usalama wa safari za anga.
Hata hivyo kumekuwa na juhudi za kuboresha safari za anga tangu kutokea misururu ya ajali za ndege mwaka 2005

Waraka Wa Godbless Lema Kwa JKIKULU ILIINGILIA KESI YA UCHAGUZI. – GODBLESS LEMA.

“ Ndugu Wananchi;

Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa ndugu zetu wa Arusha kwa kuwapokea vizuri na kuwakarimu vyema wageni wetu hao. Nawaomba waendelee na moyo huo mpaka watakapoondoka wote. Naomba kuwepo kwa mkutano huu kuwakumbushe umuhimu wa mji wenu kuwa tulivu. Miaka miwili iliyopita isingekuwa rahisi kwa watu au shirika kubwa la kimataifa kama Benki hii kuamua kufanya mkutano wake Arusha. Isitoshe hata sisi wenyewe tusingeshawishika kuomba au kukubali maombi ya namna hiyo. Lakini sasa imewezekana. Naomba kila mmoja wetu aweke azimio moyoni mwake la kuhakikisha kuwa hali ile haijirudii tena. Nyota ya Geneva ya Afrika lazima iendelee kuangaza. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo . ( J.K . KIKWETE.)

“Narudia tena , IKULU iliingilia kesi yangu ya Ubunge”.

Mh Rais nimekusikiliza kwa makini sana ila nakupa pole kwani bado unafikiri unaongea na Tanzania ya mwaka 1961 , umesema sasa Arusha ni shwari tofauti na miaka miwili iliyopita kwani sasa kuna amani na utulivu wa kutosha ndio maana hata mkutano wa AFDB umefanyika Arusha .

Mh Rais , najua IKULU iliingilia kesi yangu kama ilivyoonekana na ndio sababu hata Mkuu wa Mkoa wa Arusha wakati anaapisha Wakuu wa Wilaya alimpongeza Jaji kwa hukumu nzuri aliyowafurahisha wakati kesi hiyo iko mahakama ya Rufaa , lakini jambo moja la msingi ambalo huwezi kulitambua kwa sasa ni kuwa Haki na Ukweli haviwezi kushindwa na dhuluma, ubaya wala mamlaka , natambua wewe ni Rais na unayo mamalaka makubwa katika Taifa hili lakini vile vile nataka utambue kuwa huna mamlaka makubwa dhidi ya haki , utu na ukweli.

Mh Rais hakuna Amani Duniani inayozidi Haki na usawa ,utu na ukweli , haipo na wala haitakuwepo , ndio maana kila siku nasema ni “Afadhali Vita Inayotafuta Haki na usawa kuliko Amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa Mwanadamu “umefurahia sana mkutano uliokupa fursa ya kutoa maneno ya kebehi na kudhihirisha ila chafu iliyofanywa na Serikali yako na kujaribu kuhadaa Umma kama ilivyo kawaida ya Serikali yako na Chama chako , hata hivyo wakati huu kuna mambo ya msingi yakushughulikia zaidi ya kebehi na hadaa , Uchumi wa Nchi umeyumba, huduma za msingi za jamii zimepuuzwa, Mpasuko katika suala la Muungano na vururugu zinazoendelea Zanzibar , mfumuko wa bei hizi ni sababu chache ambazo haziwezi kuruhusu wakati huu kuwa wakati wa kebehi na mizaha isipokuwa kazi .

Mh Rais , Mama Theresa , Nelson Mandela , Martin Luther Jr na Malcom X hawakuwa Wabunge kupigania haki za Nchi yao na watu wao , sihitaji Ubunge kupigania ukweli, haki na utu , nahitaji dhamira safi , nia njema na huu utakuwa wajibu wangu mpaka nakwenda kaburini , nitakapomaliza mbio hizi najua nitapata fursa ya kutazama nyuma yangu nione nini nilifanya , ukweli nisingependa kuona vituo vya mafuta , magorofa , magari na viwanja vingi kila kona ya Nchi bali Haki ,Usawa na utu vikiwa kama nguzo ya imani ya watawala wetu watakaokuwepo, pengine sitaishi miaka mingi sana kama utachukizwa sana na waraka wangu huu kwani Polisi , Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wanakutii wewe , hata hivyo siogopi kufa kwani nisipokufa kesho , nitakufa siku moja ambayo siijui , napenda kuishi maisha marefu nimwone mke wa mtoto wangu kama itawezekana , lakini kuliko iwezekane kwa kuishi kwa hofu ni bora ishindakane kwa kuthamini haki , kwa hiyo kama utakuwa umekasirika sana , unaweza kufanya jambo lolote baya kwa kutumia mamlaka yako , niko tiyari sio kesho wala leo isipokuwa sasa hivi, najua IKULU imewazulumu watu wa Arusha Mbunge wao.

Mh Rais ninajua wazi njama zote na hasira hizi zinaweza kuwa zimetokana hasa na mkutano tuliokaa Osterbay Dar mimi na wewe kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 hata hivyo sikupuuza maongezi yetu isipokuwa nilichagua kufuata dhamira yangu na wito wangu wa utumishi wa kweli katika Jimbo langu na Nchi yangu.

Mh Rais nimekuelewa na Wananchi wamekuelewa kila mahali , wewe ni Rais unayo mamlaka makubwa na mimi ni mwananchi mamlaka yangu makubwa ni kwa mke wangu tu , sina Polisi wala Usalama wa Taifa lakini nitawaomba wanyonge wafunge na kusali tuone kama mamlaka yako inaweza kushindana na haki na ukweli .

Mh Rais “Mtu anaweza kuzini kwa siri lakini hawezi kuugua ukimwi kwa siri”Serikali na Chama cha Mapinduzi kimepuuza watu na haki zao kwa muda mrefu , lakini wakati umefika ambapo hawatapuuzwa tena hata hivyo kwa kauli yako hii naamnini haiwezi kuwafundisha kazi majaji wa mahakama ya rufaa .

“ ONLY TIME WILL TELL”.


GODBLESS .J. LEMA.

Magazeti Leo Jumatatu
 
 
Blogger Templates